Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (AS) –ABNA– Ayatollah Reza Ramezani, leo Ijumaa, tarehe (13 Novemba 2026), amehutubia katika marasimu ya asubuhi ya maombolezo ya kumbukumbu ya shahada ya Hazrat Fatima Zahra (SA), yaliyofanyika katika Msikiti wa Talibzadeh (Shuhadaa), katika Wilaya ya Rudsar.
Akitoa salamu za rambirambi kwa mnasaba wa siku za kumbukumbu ya shahada ya binti mpendwa wa Mtume Muhammad (SAWW), alisema kuwa uwepo wa waumini katika mikusanyiko ya kiroho na ibada, hususan katika siku kama hizi, ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu. Alieleza kuwa Mwenyezi Mungu huwajaalia waja Wake riziki maalumu za kiroho katika baadhi ya nyakati, ikiwemo kipindi kati ya alfajiri na adhana ya swala ya asubuhi.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS) alieleza kuwa mazingira ya kiroho ya mkusanyiko wa Dua ya Nudba, pamoja na uwepo wa wanazuoni wa dini na vijana, yana thamani kubwa. Aliongeza kuwa Mkoa wa Gilan umekuwa tangu zamani chimbuko la watu mashuhuri katika nyanja za dini na mambo ya kiroho. Pia alitaja uwepo wa wanazuoni wakubwa kama Ayatollah Muhammadi Gilani na mashahidi wa eneo hilo kuwa ni miongoni mwa baraka za imani na mikusanyiko ya kidini.
Hazrat Fatima Zahra (SA): Kielelezo kwa Wanadamu Wote Bila Kujali Jinsia au Nafasi ya Kifamilia
Mwanachama wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi (Majlisi Khubregan Rahbari), akizungumzia maisha ya miaka 18 ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa tunapopitia matukio na changamoto mbalimbali za maisha ya Bibi huyo, tangu kuzaliwa kwake hadi shahada yake, tunatambua kuwa alikuwa na shakhsia ya kipekee na kielelezo kamili kwa wanadamu wote.
Alifafanua kuwa mfano wa maisha yake hauwahusu wanawake, mabinti na akina mama pekee, bali kila mwanadamu anaweza kujifunza kutokana na mwenendo na shakhsia yake.
Akizungumzia riwaya zinazohusu nafasi ya kiroho ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa katika riwaya za Ahlul-Bayt (AS), Bibi huyo ametajwa kuwa ni Hujja ya Mwenyezi Mungu. Alinukuu kauli mashuhuri ya Imam Hassan Askari (AS):
“نحن حجج الله علی خلقه و فاطمة حجة علینا”
“Sisi ni hoja za Mwenyezi Mungu kwa viumbe Vyake, na Fatima ni hoja ya Mwenyezi Mungu juu yetu.”
Ayatollah Ramezani pia alirejelea kauli ya Imam Mahdi (AF) kuhusu Hazrat Fatima Zahra (SA), ambapo Imam huyo amemtaja kuwa kielelezo chake. Alisema kuwa pale Imam Mahdi (AF), mwenye nafasi ya juu katika mfumo wa Uimamu na Wilaya, anapomtambua Hazrat Fatima (SA) kuwa mfano wake, jambo hilo linaonyesha ukubwa wa shakhsia na nafasi ya kiroho ya Bibi huyo mtukufu.
Akizungumzia mtazamo wa Imam Khomeini (RA) kuhusu shakhsia ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alibainisha kuwa pamoja na fadhila nyingi zinazotajwa kuhusu Bibi huyo, kama vile kuwa binti wa Mtume, mke wa Amirul-Muuminin (AS), na mama wa Imam Hassan (AS) na Imam Hussein (AS), jambo muhimu zaidi ni shakhsia yake binafsi na nafasi yake ya kielimu na kiroho, ambazo zimemfanya kuwa mtu wa kipekee.
Baraka za Kauthar Katika Qur'ani Tukufu Zinatokana na Uwepo wa Hazrat Fatima Zahra (SA)
Mwanazuoni huyo wa Hawza na Chuo Kikuu, akizungumzia nafasi ya Hazrat Fatima Zahra (SA) katika tafsiri ya maarifa ya Qur'ani, alisema kuwa dhana ya Kauthar katika Qur'ani Tukufu inapata maana yake kutokana na baraka za uwepo wa Hazrat Fatima Zahra (SA). Baraka hizo zimeenea na kuathiri jamii nzima ya wanadamu.
Alieleza kuwa kinyume chake, mkondo wa Takathur na Abtar unasimama upande wa batili, na tofauti kati ya mikondo hiyo miwili inaonyesha tofauti ya njia ya haki na batili.
Katibu Mkuu huyo wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS), akizungumzia baadhi ya tafsiri za ndani za Suratul-Qadr, alisema kuwa katika baadhi ya riwaya na maelezo ya kitafsiri, Hazrat Fatima Zahra (SA) ametajwa kuwa ni ukweli halisi wa Laylatul-Qadr. Aliongeza kuwa ukuu wa shakhsia na nuru yake ni mkubwa kiasi kwamba watu kama sisi hawawezi kuuelewa kikamilifu.
Ayatollah Ramezani alisema kuwa Mtume Muhammad (SAWW) alikuwa akimpa Hazrat Fatima Zahra (SA) nafasi ya pekee. Katika mwenendo wa Mtume (SAW), imeelezwa kuwa kila Bibi Fatima (SA) alipoingia katika mkusanyiko, Mtume alikuwa akisimama kwa heshima, akimpokea na kumbusu mkono wake. Alisema kuwa mwenendo huo unaonyesha nafasi ya juu ya Bibi huyo katika mfumo wa kiroho wa Uislamu.
Aliendelea kueleza kuwa Mtume (SAWW) alikuwa akisema: “Ninapotamani harufu ya Pepo, ninanusa harufu ya Fatima.” Kauli hiyo inaonyesha ukubwa na utukufu wa kiroho wa Bibi huyo, kama ambavyo Mtume (SAW) pia alizungumzia kunusa harufu ya Pepo kupitia Imam Hassan (AS) na Imam Hussein (AS).
Hazrat Fatima Zahra (SA) Alikuwa Msaidizi wa Mtume Katika Siku Ngumu Zaidi za Utume
Ayatollah Ramezani, akirejelea mazingira ya kihistoria ya maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa Bibi huyo alizaliwa katika mwaka wa tano wa Utume, kipindi ambacho Mtume Muhammad (SAWW) alikuwa akikabiliwa na mateso na mashinikizo makubwa kutoka kwa washirikina.
Alisema kuwa Mtume wa Uislamu (SAWW) alikabiliwa na mateso makubwa zaidi kuliko Mitume wengine wa Mwenyezi Mungu. Baada ya kuanza kutangaza waziwazi ujumbe wa Uislamu, mashinikizo dhidi yake na Waislamu yaliongezeka, kiasi cha kuwatesa na kuwatenga na jamii.
Mwanachama huyo wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akizungumzia kipindi cha kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na kijamii kwa Waislamu katika bonde la Shi'b Abi Talib, alisema kuwa Hazrat Fatima Zahra (SA) akiwa mtoto alishuhudia mazingira magumu ya vikwazo na mzingiro huo. Alifafanua kuwa vikwazo hivyo havikuwa vya kiuchumi pekee, bali pia vilihusisha masuala ya kijamii, ambapo watu walikatazwa kuwasiliana na kushirikiana na Waislamu.
Ayatollah Ramezani alisema kuwa katika mwaka wa kumi wa Utume, Mtume Muhammad (SAWW) alipoteza wasaidizi wake wawili wakubwa: Hazrat Khadija (SA), ambaye aliutetea Uislamu kwa nguvu zake na mali zake zote, na Hazrat Abu Talib (AS), aliyekuwa mlinzi na msaidizi wa Mtume (SAWW). Kutokana na tukio hilo, mwaka huo ulipewa jina la Aamul-Huzn, yaani Mwaka wa Huzuni.
Aliongeza kuwa Hazrat Khadija (SA) alitumia mali yake yote katika kuusaidia Uislamu na Mtume (SAW). Alisema kuwa kujitolea kwake kifedha kulikuwa kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba mwishoni mwa maisha yake hakuwa amebakiza mali yoyote kwa ajili yake mwenyewe, na hata alikuwa na wasiwasi kuhusu sanda ambayo angezikwa nayo.
Mwanazuoni huyo aliendelea kueleza kuwa Hazrat Fatima Zahra (SA), tangu utotoni, alikuwa akishuhudia mateso na changamoto alizokuwa akipitia Mtume (SAWW), na alikuwa akimsaidia katika matukio mbalimbali. Miongoni mwa matukio hayo ni pale washirikina walipomwaga matumbo ya ngamia juu ya kichwa na uso wa Mtume (SAWW). Wakati huo, Hazrat Fatima (SA) ndiye aliyekuja na kusafisha uchafu huo usoni mwa baba yake na kumtetea Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Akizungumzia Hijra ya Mtume (SAWW) kwenda Madina na vita vya mwanzoni mwa Uislamu, alisema kuwa katika maisha yake ya miaka 18, Hazrat Fatima Zahra (SA) alishuhudia matukio mengi magumu, yakiwemo mateso dhidi ya Waislamu, mzingiro wa Shi'b Abi Talib, kufariki kwa mama yake na babu yake, njama za kumuua Mtume (SAWW), pamoja na vita vya mwanzoni mwa Uislamu. Katika hatua zote hizo, alikuwa na uwepo wenye athari na ulioambatana na uwajibikaji.
Nyumba ya Hazrat Fatima Zahra (SA): Shule ya Kulea Wanadamu Wakubwa
Ayatollah Ramezani, akizungumzia nafasi ya kifamilia na malezi ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa wakati mwingine nafasi ya mwanamke hutambulishwa kwa kuhusishwa tu na uwepo wake nyumbani, ilhali nyumba ya Hazrat Fatima (SA) ilikuwa imegeuka kuwa shule na chuo cha kulea na kujenga wanadamu.
Alisema kuwa licha ya kuwa na vifaa na uwezo mdogo wa maisha, Bibi huyo aliwalea watoto kama Imam Hassan (AS), Imam Hussein (AS), Hazrat Zainab (SA) na Hazrat Umm Kulthum (SA), ambao kila mmoja ana nafasi kubwa katika historia ya Uislamu.
Akisisitiza maisha ya kujisitiri na kuridhika na kidogo kwa Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa pamoja na nafasi yake ya juu ya kiroho, maisha yake yalipita katika hali ya kutumia mahitaji machache na kuridhika na kile kilichokuwepo. Hata wakati ambapo vifaa vya nyumbani havikutosha, alikuwa akiepuka kuomba kitu ambacho huenda Amirul-Muuminin (AS) asingekuwa na uwezo wa kukipata.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS), akizungumzia utoaji na ukarimu wa Amirul-Muuminin (AS) na Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa katika riwaya imeelezwa kuwa Amirul-Muuminin (AS), baada ya kuuza mazao ya bustani yake, aligawa mapato yote kwa watu wenye mahitaji. Aliporudi nyumbani, hakuwa amebakiza chochote kwa ajili ya familia yake. Hata hivyo, Hazrat Fatima Zahra (SA) alipokea hali hiyo bila malalamiko, kwa moyo wa kushirikiana na kuridhika.
Akizungumzia uhusiano wa kihisia na kiroho kati ya Amirul-Muuminin (AS) na Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa Amirul-Muuminin (AS) aliwahi kusema kuhusu mke wake mtukufu kwamba hakuwahi kumkasirisha wala kumfanya asimtii au kumhuzunisha. Pia alisema kuwa kila alipomtazama Hazrat Fatima (SA), huzuni na masikitiko yake yote yaliondoka.
Ayatollah Ramezani pia alizungumzia nafasi ya upendo wa baba na uhusiano wa kihisia wa Mtume Muhammad (SAW) katika maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA). Alisema kuwa baada ya kushuka kwa aya ya Qur'ani kuhusu namna ya kumwita Mtume (SAWW), ambapo Waislamu walikatazwa kumwita kwa jina lake moja kwa moja, Hazrat Fatima (SA) pia alijaribu kumwita kwa majina kama Rasulullah na Nabiyyullah. Hata hivyo, Mtume (SAWW) alimwomba aendelee kumwita kwa jina la upendo la “Baba”.
Alisisitiza kuwa nyumba ya Hazrat Fatima Zahra (SA) haikuwa mazingira ya kifamilia tu, bali ilikuwa nyumba iliyojaa upendo, mambo ya kiroho, ibada na furaha inayotokana na Mwenyezi Mungu. Ilikuwa nyumba ambayo ndani yake kulikuwa na mapenzi kwa Mwenyezi Mungu na malezi ya wanadamu wa kimungu.
Ibada na Maarifa ya Mwenyezi Mungu Vilikuwa Sifa Kuu za Maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA)
Mwanazuoni huyo wa Hawza na Chuo Kikuu, akizungumzia nafasi ya ibada katika maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa Bibi huyo alikuwa katika daraja la juu sana la maarifa na uhusiano na Mwenyezi Mungu. Ibada na kusimama usiku kwa ajili ya ibada (Tahajjud) vilikuwa sehemu isiyotenganishika na maisha yake.
Mwanachama wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akirejelea riwaya kuhusu kipindi cha utoto wa Hazrat Fatima (SA), alisema kuwa katika riwaya moja imeelezwa kuwa Mtume Muhammad (SAW) aliwahi kumuuliza kama alikuwa na haja yoyote ili amuombee kwa Mwenyezi Mungu. Hata hivyo, Bibi huyo alijibu kuwa alikuwa akizungumza na kufanya maombi ya siri kwa Mwenyezi Mungu, na hakuona inafaa kuomba kwa mwingine asiye Mwenyezi Mungu katika hali hiyo.
Ayatollah Ramezani, akizungumzia kauli ya Amirul-Muuminin (AS) kuhusu Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa alipoulizwa kuhusu namna mke wake alivyokuwa akimsaidia katika maisha, Amirul-Muuminin (AS) alimtaja kuwa msaidizi bora katika njia ya kumtii na kumuabudu Mwenyezi Mungu.
Alisema kuwa jambo hilo linaonyesha kuwa maisha ya ndoa ya watu hao wawili watukufu yalijengwa juu ya msingi wa mambo ya kiroho, maarifa na kufuata njia ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu.
Pia alizungumzia nafasi ya pekee ya Hazrat Fatima Zahra (SA) katika maarifa yanayohusiana na Ahlul-Bayt (AS), akisema kuwa Ahlul-Bayt (AS) ni njia kamili zinazomwezesha mwanadamu kupata uongofu na kufikia maarifa ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu kupitia kuwatambua na kuwafuata, anaweza kufikia ukweli wa Tauhidi na ibada ya Mwenyezi Mungu.
Mushaf wa Fatima (SA): Unaonyesha Nafasi Yake ya Pekee Katika Ulimwengu wa Ghaibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS), akizungumzia moja ya sifa za pekee za Hazrat Fatima Zahra (SA) baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (SAWW), alisema kuwa miongoni mwa daraja zinazotajwa kuhusu Bibi huyo ni kushukiwa na Malaika Jibril katika kipindi cha baada ya kufariki kwa Mtume (SAW). Alisema kuwa suala hilo pia limezungumziwa katika maelezo ya Imam Khomeini (RA).
Aliongeza kuwa baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (SAWW), Malaika Jibril alikuwa akimteremkia Hazrat Fatima Zahra (SA) ili kumfariji na kumweleza kuhusu matukio na mambo yatakayotokea siku zijazo. Amirul-Muuminin Ali (AS) alikuwa akiandika maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Jibril, na mkusanyiko wa maelezo hayo ulijulikana kwa jina la Mushaf Fatima (SA).
Ayatollah Ramezani alisisitiza kuwa Mushaf Fatima (SA) si Qur'ani nyingine, bali ni mkusanyiko wa taarifa na habari za ghaibu pamoja na matukio ya siku zijazo, ambayo yametajwa katika riwaya za Ahlul-Bayt (AS). Katika baadhi ya mapokezi, pia imeelezwa kuhusu umuhimu wa mkusanyiko huo katika kutambua matukio yajayo.
Jambo Kuu Lililokuwa Likimsumbua Hazrat Fatima Zahra (SA) Lilikuwa ni Kuiunganisha Jamii na Imam
Ayatollah Ramezani, akisisitiza ujumbe muhimu zaidi wa kisiasa na kijamii katika mwenendo wa Hazrat Fatima Zahra (SA) baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (SAW), alisema kuwa miongoni mwa mambo makuu yaliyokuwa yakimsumbua Bibi huyo ni kumtambulisha Imam na kuzuia jamii kujitenga na njia ya Uimamu.
Alieleza kuwa ili mwanadamu afikie saada, anapaswa kumtambua Imam wake, kumpenda, kumtii na kushikamana na Wilaya yake.
Akizungumzia nafasi ya Amirul-Muuminin (AS) katika mfumo wa uongofu wa Kiislamu, alisema kuwa Amirul-Muuminin (AS) ndiye mlango wa elimu na hekima, na njia ya kuingia katika maarifa ya Mwenyezi Mungu. Mwanadamu anapaswa kupitia njia ya Ahlul-Bayt (AS) ili kufikia ukweli wa dini. Hazrat Fatima Zahra (SA), kupitia mwenendo na misimamo yake, alikuwa akiiita jamii kumtambua na kumfuata Imam.
Akirejelea Hadithi isemayo “Aliyyun ma'al-Haqq wa al-Haqqu ma'a Ali” (Ali yuko pamoja na haki na haki iko pamoja na Ali), alisema kuwa uhusiano kati ya Amirul-Muuminin (AS) na ukweli ni uhusiano usioweza kutenganishwa. Maana yake ni kwamba haki iko pamoja na Ali (AS), na popote Ali (AS) alipo, ukweli na haki pia vipo katika njia hiyo.
Mwanazuoni huyo wa Hawza na Chuo Kikuu, akizungumzia nafasi ya Uimamu katika kuiongoza jamii, alisisitiza kuwa kujitenga na Imam kunatengeneza mazingira ya upotovu wa kimawazo na kimaadili. Jamii inapaswa kudumisha uhusiano wake na Imam ili iweze kufikia saada.
Alisema kuwa suala hilo linaonekana pia katika zama za sasa kupitia suala la Wilaya ya Faqih na kupambana na dhuluma pamoja na kuwaunga mkono watu wanaodhulumiwa.
Aliongeza kuwa Hazrat Fatima Zahra (SA) alikuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa jamii ya Kiislamu na hali ambayo Amirul-Muuminin (AS) angekabiliwa nayo baada ya kufariki kwake. Bibi huyo alikuwa na hofu kuhusu matukio ambayo yangewakumba Ahlul-Bayt (AS) baada yake, na alijitahidi kuwaunganisha watu na njia ya Uimamu pamoja na Kamba ya Mwenyezi Mungu, ili wasipotee kutoka katika njia ya saada.
Mwenendo wa Hazrat Fatima Zahra (SA): Mchanganyiko wa Ibada, Kujitolea na Uwajibikaji wa Kijamii
Ayatollah Ramezani, akirejelea aya za Suratul-Insan na tukio la nadhiri ya Imam Hassan (AS) na Imam Hussein (AS), alisema kuwa katika maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA) na Amirul-Muuminin (AS), kujitolea na kutoa sadaka kulikuwa na nafasi kubwa, hata katika mazingira ambayo familia ilikuwa ikikabiliwa na uhaba wa mahitaji.
Alieleza kuwa chakula kidogo cha familia hiyo wakati wa kufuturu kilikuwa kikitolewa kwa masikini, yatima na mateka, kwa lengo la kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu.
Alisisitiza kuwa mwenendo wa Hazrat Fatima Zahra (SA) unaonyesha kuwa mwanadamu anaweza, hata anapokabiliwa na changamoto za maisha, kudumisha ibada kwa Mwenyezi Mungu, kujitolea, uwajibikaji na kuwajali wengine kwa kiwango cha juu. Sifa hizo ndizo zinazomfanya Bibi huyo kuwa kielelezo cha kudumu kwa wanadamu wote.
Mwisho, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (AS), akizungumzia siku za mwisho za maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA) na dhuluma alizokumbana nazo, alisema kuwa katika mapokezi ya kihistoria imeelezwa kuwa baada ya kufariki kwa Mtume Muhammad (SAWW), Bibi huyo alipitia siku ngumu sana.
Alisema kuwa katika kipindi hicho, alitabasamu katika matukio mawili tu: la kwanza, aliposikia habari kuwa muda wa kuungana tena na Mtume (SAWW) ulikuwa umekaribia; na la pili, alipopata uhakika kuhusu namna mwili wake mtukufu utakavyofunikwa ndani ya jeneza.
Mwakilishi wa wananchi wa Gilan katika Baraza la Wanazuoni Wataalamu wa Uongozi, akisisitiza umuhimu wa kuchunguza upya vipengele mbalimbali vya maisha ya Hazrat Fatima Zahra (SA), alisema kuwa kuutambua mwenendo wa Bibi huyo kunapaswa kusababisha uelewa wa kina zaidi wa maarifa ya Ahlul-Bayt (AS), kuimarisha uhusiano na Imam na kufuata njia ya kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Alisisitiza kuwa njia ya saada ya mwanadamu inapitia katika kuwatambua na kushikamana na Hujja wa Mwenyezi Mungu.
Maoni yako